Masha, wafuasi wa Lowassa watupwa Segerea
SIKU moja baada ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Laurence Masha, kukamatwa na kulazwa kwenye Kituo cha Polisi Oysterbay, jijini Dar es Salaam, amefikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka kisha kupelekwa katika Gereza la Segerea.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, Masha alikamatwa juzi jioni baada ya kufika Kituo cha Polisi Osterbay, kwa lengo la kuwadhamini vijana 19 waliokuwa wamekamatwa kwa madai ya kukusanyika kinyume cha sheria.
Vijana hao wanadaiwa kuwa ni wafuasi wa mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, kutoka kundi la 4U Movement.
Wakiwa wamevaa fulana zilizoandikwa ‘Team Mabadiliko’, vijana hao walikuwa eneo la makutano ya barabara ya Kawawa, Mwai Kibaki, Alhasan Mwinyi na New Bagamoyo.
Jana, Masha na wenzake 19, wakiwamo wanafunzi 10 na wafanyabiashara tisa, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya mahakimu wawili tofauti.
Wakati vijana hao wakishtakiwa kwa tuhuma za kula njama na kufanya mkusanyiko usio halali, Masha ameshtakiwa kwa kutoa lugha ya matusi na vitisho kwa maofisa wa polisi katika Kituo cha Polisi Oysterbay.
Wakili wa Serikali, Wankyo Simon, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Waliarwande Lema, alidai kuwa mshtakiwa Masha anakabiliwa na shtaka moja.
Simon alidai kuwa Agosti 24, mwaka huu, katika Kituo cha Polisi Oysterbay, Masha alitumia lugha ya matusi na vitisho kwa Inspekta Msaidizi wa Polisi, Juma Mashaka na polisi wengine.
Inadaiwa aliwaambia polisi hao ni ‘stupid’, washenzi, waonevu, hawana shukurani, huruma wala dini, maneno ambayo yalisababisha uvunjifu wa amani.
Masha alikana mashtaka, upelelezi haujakamilika na upande wa Jamhuri haukuwa na pingamizi kwa mshtakiwa kudhaminiwa.
Hakimu Lema alikubali mshtakiwa kudhaminiwa kwa dhamana ya Sh milioni moja na wadhamini wawili ambao watasaini dhamana ya Sh milioni moja. Wadhamini walikuwapo lakini mahakama iliamuru barua zao kufanyiwa uhakiki.
Amri ya kufanyiwa uhakiki kwa barua hizo ilitolewa saa tisa mchana wakati mshtakiwa huyo alipomaliza kusomewa mashtaka.
Hata hivyo, Masha alifika mahakamani hapo saa nne asubuhi na kuwekwa mahabusu hadi muda huo aliosomewa mashtaka.
Kwa kuwa sharti hilo la uhakiki halikuweza kutimizwa jana, mshtakiwa alipelekwa mahabusu katika Gereza la Segerea. Kesi itatajwa Agosti 7 mwaka huu.
Kwa upande wa wanafunzi 10 na wafanyabiashara tisa, walisomewa mashtaka na Wakili wa Serikali, Paul Kadushi mbele ya Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru.
Washtakiwa hao waliovalia tisheti zilizoandikwa ‘Team Mabadiliko, mabadiliko yasipopatikana ndani ya CCm yatapatikana nje ya CCM’ ni Rwegasira Alex (23), Yusuph Adam (22), Sia Kimambo (21), Mariamu Michael (20), Jackline Michael (25), Edwina Kaiza (25), Dickoson Congress (25), Mary Malick (30), Jumanne Mvuma (28) na Francis Mbwilo (22).
Wengine ni Michael Litanda (25), Vian Nchimbi (25), Scolastika Masanja (29), Pradius Kaiza (29), Godfrey Mhando (25), Abdalla Hamisi (28), Fortune Francis (20), Baraka Athuman (22) na Saidi Katora (30).
Kadushi alidai washtakiwa hao kwa pamoja Agosti 24, mwaka huu, maeneo yasiyojulikana jijini Dar es Salaam, walikula njama ya kutenda kosa la kukusanyika isivyo halali.
“Mheshimiwa shtaka la pili, washtakiwa wote kwa pamoja Agosti 24, mwaka huu maeneo ya Morocco, Dar es Salaam, walikusanyika bila kibali kwa lengo ka kufanya maandamano na kusababisha watu wa maeneo hayo kuamini kungetokea uvunjifu wa amani,” alidai.
Washtakiwa wote walikana mashtaka, upelelezi haujakamilika na upande wa Jamhuri haukuwa na pingamizi kwa kupewa dhamana.
Wakili wa utetezi, Peter Kibatala aliomba washtakiwa wapewe masharti nafuu kwa sababu tangu juzi walikuwa polisi na mashtaka yanayowakabili ni ya kawaida.
Hakimu Mchauru aliwataka washtakiwa kuwa na wadhamini wawili kila mmoja wanaofanya shughuli zinazotambulika, wasaini dhamana ya maandishi ya Sh 800,000 na washtakiwa hawatakiwi kutoka nje ya Dar es Salaam bila kibali cha mahakama.
Washtakiwa walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na walirudishwa rumande hadi Septemba 8, mwaka huu kesi itakapotajwa.
Wakati wa kupelekwa gerezani saa kumi alasiri, Masha na wenzake walisindikizwa na msafara wa magari manane ya polisi pamoja na gari kubwa lenye maji ya kuwasha, huku king’ora kikipigwa.
Akizungumza na gazeti hili kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Camilius Wambura, alisema vijana hao walikamatwa saa 12 wakiwa katika mkusanyiko aliosema haukuwa kihalali kisheria.
“Polisi walivyowataka kutawanyika waligoma. Kutokana na hali hiyo, polisi walitumia maarifa kuwatawanya na kufanikiwa kuwakamata vijana 19,” alisema Kamanda Wambura.
Wambura alisema baada ya vijana hao kukamatwa, Masha alifika kituoni hapo na kuwataka polisi kuwaachia huru.
“Baada ya askari polisi kugoma kutii amri yake, alianza kuwatolea maneno yasiofaa na kutoa salamu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiwa hapo hapo mapokezi. Alikuwa anasema ‘Peoples…’ ndipo wakamkamata na kumuweka ndani,” alisema.
Jana asubuhi, gazeti hili lilishuhudia ulinzi mkali katika Kituo cha Polisi Oysterbay ambapo watu walikuwa hawaruhusiwi kukaribia eneo hilo.
Pia kulikuwa na magari matano yaliyokuwa yamejaa askari waliokuwa na silaha za moto.
Ilipofika saa 4:37 asubuhi, Masha na vijana hao waliondolewa kituoni hapo wakiongozwa na gari ya king’ora na mengine matatu ya polisi aina ya Land Cruiser kwenda Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo walifika saa 4:45.
0 comments Blogger 0 Facebook
Post a Comment