Je unapenda mihogo ? Mie pia napenda sana mihogo, hasa mihogo ya
kuchoma, ikiwa na pilipili na kachumbari yenye limao la kutosha. Kuna
nini kingine kinaweza kuzidi ladha hii tamu?
Mihogo ni chakula kikuu katika kanda nyingi za nchi za tropiki. Pia,
mihogo hustawi vizuri sehemu kame kutokana na kutohitaji maji mengi.
Mihogo pia ni chanzo kikubwa cha wanga kwa bei nafuu, hasa kwa nchi za
kusini mwa jangwa la sahara. Mihogo hutumika kama chakula – ugali wa muhogo na kutengeneza bidhaa tofauti – chips, mihogo ya kukaanga, kuchemsha n.k.
Kwa muda mrefu tafiti
tofauti zinaonyesha madhara ya mihogo kwa maisha ya walaji wake, hasa
wale wasiofanya maandalizi mazuri kabla ya kula chakula hiki. Tafiti
zinaoyesha kuwa mihogo ina kemikali mbili aina cyanogenic glucosides, zinazoitwa linamarin na lotaustralin. Hizi kemikali pamoja na kimeng’enyo kinachoitwa linamarase, ambacho hupatikana pia kwenye mihogo, huyeyushwa mwilini na kutengeneza kemikali aina ya Cyanide. Cyanide ni sumu ambayo uwepo wake kwa kiasi kidogo mwilini huweza kuleta madhara makubwa ya afya na hata kusababisha kifo.
Aina za mihogo
Mihogo inaweza kutengwa kwenye makundi makuu mawili – mihogo mitamu na mihogo michungu. Mihogo mitamu ina kiwango kidogo sana cha kemikali hatarishi za cyanogenic glucosides. Hivyo, mara nyingi haina madhara makubwa kama ikiandaliwa vizuri kabla ya kuliwa.
Mihogo michungu ina kiwango kikubwa cha kemikali za cyanogenic glucosides.
Uwingi wa hizi kemikali ndio hufanya mihogo hii kuwa michungu zaidi.
Hii ni aina ya mihogo inayohusishwa moja kwa moja na madhara ya afya na
vifo vinavyotokana na sumu ya cyanide. Mihogo michungu hustawi zaidi
sehemu zilizo kame.
Kiwango cha sumu kwenye mihogo
Kiwango cha sumu kilichopo kwenye mihogo hutofautiana. Mihogo mitamu
huweza kutoa kiasi cha miligramu 20 za Cyanide kwa kila kilo 1 ya muhogo
mbichi. Mihogo michungu hutoa kiasi zaidi ya mara 50 ya hiki kwa kila
kilo ya muhogo mbichi – yaani gramu 1 kwa kila kilo 1 ya muhogo mbichi.
Fahamu kuwa, kiasi cha miligramu 25 cha cyanide toka kwenye muhogo
mbichi inatosha sana kumuua panya. Uwingi wa sumu hii huweza kumuathiri
vibaya sana binadamu kwa kuharibu mfumo wa fahamu na kumpa ugonjwa wa
kupooza unaoitwa Konzo.
Watoto wadogo wako kwenye hatari zaidi ya kuathirika na mihogo kuliko
watu wazima sababu ya udogo wa miili yao kulinganisha na kiwango cha
sumu wanayoweza kula kwenye mihogo. Ni muhimu kuwa makini na kila kitu
kinachoweza kupewa mtoto kiandaliwe vizuri, na kupunguza idadi ya vitu
vibichi ambavyo mtoto anaweza kula – hasa vyakula vya mizizi kama
mihogo.
Jinsi ya kuepuka madhara
Nafahamu wengi tumekulia kwa kula mihogo miaka mingi sana, iwe shule au nyumbani, mibichi au ya kupikwa, kawaida au kama unga.
Lakini hizi siyo sababu za kupinga utafiti uliothibitishwa. Ili kuweza
kulinda afya zetu, za watoto wetu na wale tunaowapenda, hizi hapa njia
chache kati ya nyingi zinazoweza kutumika katika kuandaa mihogo vizuri
ili kuzuia madhara ya sumu ya mihogo.
1. Usile migoho mibichi
Kuna baadhi ya watu huamini kuwa kula mihogo mibichi huwaongezea
nguvu za kiume. Kuna watu wengi huuza mihogo mibichi barabarani na wengi
hununua. Mie binafsi sijathibitisha hilo la nguvu za kiume, lakini
kutokana na utafiti huu inaonyesha kuwa mihogo huwa na madhara makubwa
zaidi ya kiafya kama ikiliwa mibichi. Hivyo ni vizuri kuzingatia ushauri
wa kufuata kanuni bora za kuandaa chakula ili kiwe afya badala ya
madhara mwilini.
Kwa mtu mwenye mahitaji ya kuongeza nguvu za kiume kwa kutumia
vyakula, kuna makala inayohusiana na hivi vyakula ambavyo ni salama
kabisa. Unaweza kusoma hapa.
2. Andaa mihogo vizuri
Jamii tofauti zinazotumia mihogo kama chakula kikuu huelewa umuhimu
wa maandalizi bora ya mihogo ili kuepuka madhara yake. Wengi hutumia
mbinu za kuloweka, kuanika na kupika kwa muda mrefu kabla ya kuwa tayari
kuliwa. Kuloweka mihogo au kuanika juani hufanya sumu iliyomo kuondoka
na mihogo kuwa salama kuliwa.
3. Usile Maganda
Kiasi kikubwa sana cha sumu ya mihogo imejaa kwenye maganda. Ulazi wa
maganda ya mihogo, kwa binadamu au wanyama, huwa na madhara makubwa au
hata kifo. Hakikisha maganda yanatupwa na kukaa mbali na mifugo na
watoto ambao wanaweza kula bila kujua.
0 comments Blogger 0 Facebook
Post a Comment